Advertising

KABLA YA UJAUZITO, UJAUZITO NA LISHE

KABLA YA UJAUZITO, UJAUZITO NA LISHE

Ni nadra kwa familia nyingi katika nchi zinazoendelea kuwa na maandalizi kabla ya mama kuwa mjamzito. Maandilizi haya ni muhimu sana kwa kuwa yatachangia afya ya baadae ya mama na mtoto na kupelekea kuwa na familia yenye furaha.
Ni muhimu sana kwa mwanamama anayetegemea kuwa mjamzito kubadili tabia mbalimbali kama unywaji wa pombe, uvutaji wa sigara, kuepuka vinywaji vyenye kafeini, matumizi ya aina mbali mbali ya dawa na hata utumiaji wa dawa za kulevya. Kubadili tabia kutakuwa na faida kubwa endapo mama anategemea kuwa mjamzito. Matumizi ya vinywaji vilivyotajwa pamoja na matumizi ya tumbaku na dawa za kulevya huathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa mtoto aliye tumboni, hasa katika awamu ya kwanza ya ujauzito (first trimester) kwa kuwa ndio wakati ogani za mtoto kama ubongo na nyinginezo zinakuwa zinatengenezwa. Kwa hiyo ni muhimu mama kuzingatia na kumuepusha mtoto na ulemavu.
Afya njema kwa ujumla, lishe bora pamoja na mazoezi ya
mwili ni vitu muhimu vya kuzingatia endapo unategemea kuwa mjamzito. Kuwa na mipango kabla ya kupata ujauzito, pia mtembelee daktari wako. Ongea na daktari wako kuhusu mtindo wa maisha( life style ), lishe unayotumia, dawa, vitamini na hata historia yako kiafya na historia ya familia na pia lolote lile unalofikiri ni muhimu daktari wako kufahamu. Daktari wako atakushauri kuhusu jinsi ya kujihudumia kabla ya kupata ujauzito, chanjo yeyote kama itahitajika kabla ya ujauzito. Pia mwanamama kutibiwa endapo atakuwa na tatizo lolote la kiafya ambalo linaweza kumwathiri mama na mtoto wakati wa ujauzito.
Mwanamama ajitahidi kuuweka mwili wake katika hali njema kiafya, aepuke vinywaji kama pombe na vyenye kafeini, pia matumizi ya madawa ya kulevya. Ajitahidi kuwa na uzito unaotakiwa, pia kama ana ugonjwa wa kisukari aakikishe anafuata masharti na afanye mazoezi angalau muda wa nusu saa kwa siku, ale kwa wingi matunda, mboga za majani na nafaka isiyokobolewa. Maandalizi haya yawe ni miezi mitatu kabla katika mwaka unaotegemea kuwa mjamzito.
Unapopata ujauzito, chakula bora ni muhimu sana kupita maelezo. Unahitajika kula vyakula vyenye virutubisho kwa wingi zaidi kama protini, madini ya chuma, kalshamu na folic acid ukilinganisha na wakati ambao haukuwa na ujauzito. Pia unahitaji vyakula vinavyoongeza nguvu nishati (calories). Lakini “kula kwa ajili ya wawili” haimaanishi kula mara mbili zaidi ukilinganisha na wakati ambao haukuwa na ujauzito. Ila inamaanisha kula chakula cha kutosha chenye virutubisho muhimu kwa ajili yako na mtoto anayekua tumboni.
Ni kawaida kwa mama mjamzito kuongezeka uzito kwa nyakati tofauti za ujauzito, lakini mara nyingi uzito huongezeka zaidi katika awamu ya mwisho ya ujauzito ( third trimester).
   
Aina ya virutubisho vya vyakula kwa mjamzito
Protini
Protini katika chakula cha mama mjamzito inasaidia ukuaji wa tishu za mtoto, hiyo ni pamoja na ubongo pia hata ogani nyingine za mwili. Pia inasaidia matiti na tishu za tumbo la uzazi kukua wakati wa mimba, na pia inachangia usambazaji mzuri wa damu. Mama anahitajika kula milo 2 hadi 3 kwa siku yenye vyakula vya protini kama vifuatavyo:-
  • Nyama ya ng’ombe ya steki.
  • Samaki wa maji baridi au maji chumvi.
  • Maini.
  • Nyama ya kondoo
  • Karanga au aina nyingine za nati.
  • Jamii ya mikunde kama maharage.
Kalshamu (Calcium)
Mama mjamzito anahitaji madini ya kalshamu kama miligramu 1000 kwa siku. Madini ya kalshamu yanasaidia kurekebisha viwango vya majimaji mwilini, kujenga mifupa na meno ya mtoto aliye tumboni. Vyakula vyenye madini haya ni kama:-
  • Mayai.
  • Maziwa
  • Jibini
  • Maharage meupe
  • Maharage ya soya
  • Samaki
  • Kabichi
Madini ya chuma
Madini ya chuma husaidia kuongeza kiwango cha damu mwilini na kukukinga na upungufu wa damu mwilini (Anemia). Vyakula vyenye madini ya chuma ni kama vifuatavyo:-
  • Spinachi
  • Mchicha
  • Kabichi
  • Nyama
  • Maini
  • Nafaka zisizokobolewa
  • Samaki
  • Mayai
Folic acid
Folic acid acid hupatikana katika vyakula tunavyokula, hii husaidia kujengeka vizuri kwa ogani za mtoto na kumuepusha na ulemavu pamoja na tatizo linalojulikana kitaalam kama mgongo wazi au neural tube defect (NTD). Katika nchi zinazoendelea mara nyingi wajawazito huwa hawapati virutubisho hivi kwa kiasi cha kutosha katika vyakula, kwa hiyo kinamama wajawazito huongezewa virutubisho hivi kama vidonge vya folic acid wanapohudhuria kliniki. Folic acid hupatikana katika vyakula kama:-
  • Kabichi
  • Spinachi
  • Machungwa
  • Papai
  • Limao
  • Embe
  • Nyanya
  • Zabibu
  • Tikiti
  • Nafaka
  • Mkate
  • Jamii za mikunde kama maharage
Vitamini C
Matunda na mbogamboga huwa na vitamini C kwa wingi. Vitamini C husaidia uponaji wa majeraha kwa haraka, husaidia meno na fizi na kujengeka kwa mifupa, pia husaidia mmeng’enyo. Vyakula vyenye vitamini C ni kama:-
  • Machungwa
  • Limao
  • Nyanya
  • Zabibu
  • Pilipili
  • Embe
  • Mboga za majani
Tahadhari
Mama mjamzito anatakiwa kuhakikisha kuwa vyakula vyote hivi, lazima viandaliwe katika mazingira safi kuepuka athari kwa mama na mtoto. Vyakula vingine visipopikwa vizuri vyaweza kuwa na vimelea hatari vya magonjwa kama Salmonella na E coli pia aina nyinginezo za vimelea ambavyo vyaweza kuwa hatari kwa afya.
Mpango wa mazoezi
Mpango wa mazoezi ni muhimu kwa mama mjamzito kwa kuwa mazoezi husaidia maendeleo ya kiafya ya mama na mtoto aliye tumboni.Pia mazoezi humsaidia mama kuwa mwenye nguvu wakati wa kujifungua. Mazoezi ya kutembea huwafaa sana kina mama walio wajawazito. Lakini ni vyema kushauriana na daktari wako kabla ya kujihusisha na aina yeyote ya mazoezi.
KABLA YA UJAUZITO, UJAUZITO NA LISHE KABLA YA UJAUZITO, UJAUZITO NA LISHE Reviewed by Unknown on 12:38 PM Rating: 5

No comments:

Events

Powered by Blogger.